Mkutano wa tatu wa kilele wa ushirikiano wa kimataifa wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” umefanyika hivi karibuni mjini Beijing, na kuwashirikisha takriban wajumbe 10,000 kutoka nchi 151 na mashirika 41 ya kimataifa, wakiwemo viongozi wa nchi na mashirika 20 ya kimataifa.
Ikiwa mmoja wa washiriki muhimu zaidi, Afrika inakaribisha ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, na pendekezo hilo limepata mafanikio makubwa, na kuonesha uhai mkubwa barani humo.
Mwaka 2013, Rais Xi Jinping wa China alitoa pendekezo la kujenga kwa pamoja “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, ili kuhimiza maendeleo ya pamoja ya nchi mbalimbali duniani. Hadi sasa, pendekezo hilo limeshirikisha zaidi ya nchi 150 duniani, zikiwemo nchi 44 za Afrika zilizoko kusini mwa Jangwa la Sahara. Nchi hizo za Afrika na China zimeendelea kuimarisha ushirikiano wao kufuatia pendekezo hilo, na kuwa mfano wa kuigwa kwa ushirikiano kati ya nchi za Kusini.
Kutokana na pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, China imezisaidia nchi za Afrika kujenga zaidi ya kilomita 6,000 za reli, kilomita 6,000 za barabara, karibu bandari 20 na zaidi ya vituo vikubwa 80 vya umeme katika miaka 10 iliyopita. Takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” ni muhimu kwa Afrika kuboresha miundombinu na kuhimiza maendeleo ya uchumi.
Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” linaendana na mipango na mikakati ya maendeleo ya nchi za Afrika. Kwa mfano, “Agenda ya 2063” ya Umoja wa Afrika inataka kutatua upungufu wa miundombinu na kukuza ushirikiano wa uchumi barani Afrika. Kufuatia pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, China na nchi za Afrika zimeshirikiana kujenga miradi mingi mikubwa ya miundombinu barani Afrika, ambayo imehimiza mawasiliano ya nchi za bara hilo. Aidha, “Ajenda ya 2063” inatetea kujenga eneo la biashara huria barani Afrika, lakini haiwezekani kujenga soko la pamoja, bila mtandao kamilifu wa miundombinu. Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” pia linasaidia kutatua tatizo hilo.
Ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” unakaribishwa kidhati na nchi za Afrika. Rais William Ruto wa Kenya aliyehudhuria mkutano huo amesema, kupitia ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, Kenya na China zimeimarisha uhusiano wao, na kuanzisha kwa pamoja “mfumo mkubwa wa ikolojia” wenye urafiki na ushirikiano zaidi.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed anaona kuwa pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” limekuza biashara kati ya nchi za Afrika na biashara kati ya Afrika na China, kuleta ajira nyingi na kukuza maendeleo ya uchumi barani Afrika.
Rais Denis Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Kongo amesema pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” limechangia maendeleo ya Afrika, na utekelezaji wa pendekezo hilo umeboresha kwa kiasi kikubwa miundombinu barani Afrika, na kuhimiza ujenzi wa eneo la biashara huria barani Afrika.