Idadi ya watalii waliofika Afrika Mashariki yatarajiwa kufika milioni 14.5 hadi 2025
2023-11-23 23:08:08| cri

Watalii wanaowasili katika eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanatarajiwa kuongezeka na kufikia rekodi ya milioni 14.5 ifikapo 2025. Jumuiya ya Afrika Mashariki imetaja kufufuka haraka kwa sekta ya utalii baada ya janga la Covid-19, kunatokana na uwepo wa bidhaa anuwai za utalii.

Idadi hii itakuwa ni ongezeko la zaidi ya mara mbili ya idadi ya wageni wanaotembelea eneo hilo, ambao mwaka 2019 walifikia milioni 7.2 kabla ya kuzuka kwa Covid-19. Mwelekeo wa kuongezeka kwa idadi hiyo ulitangazwa mjini Nairobi na Bi Annette Ssemuwemba ambaye ni naibu katibu mkuu wa EAC (Forodha, Biashara na Masuala ya Fedha).

Wakati wa janga la Covid-19 mwaka 2020/21, eneo lilipoteza zaidi ya dola bilioni 4.8 na ajira milioni mbili katika sekta ya utalii. Idadi ya watalii waliofika katika eneo hilo ilipungua kutoka milioni 6.9 kabla ya janga hilo hadi milioni 2.2 mwaka 2020, na kusababisha hasara kubwa zaidi kulikumba eneo hilo.