Mkutano wa soko la hisa wa Afrika kuboresha soko la biashara ya mitaji linalovuka mipaka
2023-11-24 09:48:52| CRI

Wawakilishi kutoka sekta ya soko la hisa barani Afrika wamekutana katika mkutano wa siku mbili ulioanza jana jijini Nairobi, Kenya, kwa lengo la kuboresha biashara ya hisa ya kuvuka mpaka kwa kampuni zilizoorodheshwa.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 26 wa Mwaka wa Shirikisho la Soko la Hisa la Afrika (ASEA), rais wa Kenya William Ruto amesema biashara ya soko la hisa za kampuni zilizoorodheshwa kati ya nchi za Afrika itawezesha kuongeza idadi kubwa ya wawekezaji katika soko la mitaji barani humo, na kuongeza kuwa, biashara hiyo pia itawezesha nchi mbalimbali kujifunza njia bora za kazi ndani ya mfumo mmoja wa kiuchumi.

Katika mkutano huo, washiriki watatafuta suluhisho thabiti la changamoto zinazoikabili sekta hiyo, na kuwezesha kuwa na mfumo wa kiuchumi wa soko la fedha la Afrika ambalo ni jumuishi na imara.