UNECA yasema kuongeza uzalishaji ni muhimu katika kukabiliana na ongezeko la kasi la idadi ya watu barani Afrika
2023-11-24 09:50:44| CRI

Tume ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa (UNECA) imetoa wito kwa nchi za Afrika kukumbatia teknolojia za kidijitali, kuboresha maingiliano ya kibiashara ndani ya bara hilo na kuwa na mfumo wa sera bora za ardhi ili kukabiliana na mahitaji ya kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya watu na ukuaji wa miji barani Afrika.

Katibu Mkuu wa UNECA, Claver Gatete amesema katika taarifa yake kuwa, kutokana na ongezeko la idadi ya watu na ukuaji wa kasi wa miji, sekta ya chakula itaendelea kukua katika miaka ijayo, na kwamba uwekezaji katika uwezo wa wakulima kuongeza uzalishaji ni hatua ya muhimu kuzingatiwa.

Pia ameeleza umuhimu wa uwekezaji katika taasisi za utafiti ili kuendeleza mifumo sahihi na endelevu ya mchakato wa kilimo, uvumbuzi wa kiteknolojia, na utekelezaji wa sera sahihi za ardhi na kilimo.

Akizungumzia Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFTA), Bw. Gatete amesema kama utekelezaji wake ukifanyika vizuri, eneo hilo lina uwezo wa kuondoa watu milioni 30 kutoka kwenye umasikini uliokithiri, kuongeza kipato cha Afrika kwa dola za kimarekani bilioni 450, huku likiwanunganisha watu bilioni 1.3.