Uhusiano kati ya VVU/UKIMWI na ulemavu ni suala ambalo linatia wasiwasi sana kwani watu wenye ulemavu mara nyingi wanakuwa kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa VVU. Zaidi ya hayo, kuna mtazamo unaozidi kuongezeka kwamba watu wanaoishi na VVU au UKIMWI pia wako katika hatari ya kuwa walemavu wakudumu au kwa muda kutokana na hali zao. Kama mtu mwingine yeyote yule, watu wenye ulemavu wanahitaji taarifa kuhusu VVU/UKIMWI na upatikanaji wa programu, huduma, na rasilimali. Katika nchi nyingi, hali ya watu wenye ulemavu inachangiwa zaidi na vikwazo vya kijamii vinavyozuia ushiriki wao kamili na mzuri katika jamii, ikiwa ni pamoja na kupata elimu.
Licha ya kuongezeka kwa uhusiano kati ya VVU/UKIMWI na ulemavu, watu wenye ulemavu bado hawajapata uangalizi wa kutosha wa kitaifa katika kupambana na VVU na UKIMWI. Zaidi ya hayo, mipango iliyopo ya kuzuia VVU, matibabu, huduma na usaidizi kwa ujumla inashindwa kukidhi mahitaji yao maalumu. Watu wenye ulemavu mara nyingi hawajumuishwi katika elimu, kinga na huduma za usaidizi za VVU kwa sababu ya kudhaniwa kuwa hawafanyi ngono au hawajihusishi katika tabia nyingine hatarishi kama vile matumizi ya dawa za kulevya.
Watoa huduma za afya ya jinsia na uzazi wanaweza kukosa maarifa kuhusu masuala ya ulemavu, au kuwa na mitazamo isiyo sahihi au ya unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu. Huduma zinazotolewa katika zahanati, hospitali na katika maeneo mengine zinaweza zisifikiwe, au kukosa vifaa vya lugha ya ishara ama hata kushindwa kutoa maelezo katika miundo mbadala kama vile Hati nundu, sauti au lugha rahisi. Katika maeneo ambayo kuna ufikiaji mdogo wa dawa, watu wenye ulemavu wanaweza kuchukuliwa kuwa kipaumbele cha chini cha matibabu. Hivyo kwa kuwa jana tarehe Mosi ilikuwa siku ya Ukimwi duniani na kesho tarehe 3 itakuwa siku ya walemavu, katika kipindi cha ukumbi wa wanawake leo tutaangalia Changamoto za walemavu walioathirika na UKIMWI na jinsi wanavyotengwa katika vita dhidi ya ukimwi.