Kenya yaanza kubinafsisha mashirika 11 ya kiserikali ili kuongeza mapato
2023-11-28 08:38:52| CRI

Serikali ya Kenya jana Jumatatu ilianza mchakato wa kubinafsisha mashirika 11 yanayomilikiwa na serikali, kwa lengo la kuongeza mapato na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika sekta mbalimbali.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango ya Kenya, imesema ubinafsishaji na urekebishaji huo unaendana na juhudi za kuelekea kuimarisha usimamizi wa kifedha na kuhimiza ukuaji wa uchumi.

Mashirika yanayotajwa kubinafsishwa ni pamoja na Kampuni ya Mafuta ya Kenya (NOCK) inayojishughulisha na utafutaji wa mafuta, uagizaji na uuzaji wa bidhaa za mafuta yaliyosafishwa, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC), kinachohimiza utalii wa mikutano, na Kampuni ya Kenya Pipeline inayodhibiti usafirishaji wa gesi na mafuta.