Afrika Kusini yajiondoa kwenye zabuni ya kuandaa Kombe la Dunia la Wanawake 2027
2023-11-28 11:01:33| cri

Afrika Kusini imejiondoa katika kinyang'anyiro cha kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la Wanawake 2027, ikieleza inahofia kwamba watalazimika "kuwasilisha mipango haraka" kwa FIFA mwezi Disemba.

Tarehe ya mwisho ya kuwasilisha mipango ya kina ya mashindano hayo ni Disemba 8 na maafisa wa Afrika Kusini wanaamini kuwa itakuwa busara zaidi kujaribu kuandaa mashindano yanayofuata ya mwaka 2031.

Mtendaji mkuu wa Chama cha Soka cha Afrika Kusini Lydia Monyepao amebainisha kuwa wameona ni bora kuwasilisha zabuni iliyoandaliwa vizuri kwa mwaka 2031, badala ya kuwasilisha mipango ya haraka.

Kujiondoa kwa Afrika Kusini kunapunguza idadi ya zabuni za kuwania kuandaa mashindano ya 2027 hadi tatu, zile zinazoandaa kwa pamoja ambazo ni Ubelgiji, Uholanzi na Ujerumani, na Mexico na Marekani, na moja kutoka Brazil.

Mkutano wa FIFA wa Mei 17, 2024 utaamua ni zabuni gani itafaulu na kufuata wenyeji wenza Australia na New Zealand katika kuandaa michuano hiyo ya kila miaka minne inayozidi kuwa maarufu.

Hispania ndio mabingwa wakiwa wameishinda Uingereza 1-0 katika fainali iliyotazamwa na umati wa watu 75,784 mjini Sydney Agosti mwaka jana.