Tanzania na China zaahidi kuimarisha ubora wa TVET
2023-11-28 23:00:04| cri

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Tanzania imesema ushirikiano kati ya Tanzania na China unatarajiwa kuongeza ubora wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET) na kuzalisha wahitimu wengi wenye uwezo wa kufanya kazi katika sekta mbalimbali za uchumi.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa Semina ya Mabadilishano ya Kitaaluma kati ya China na Tanzania kuhusu marekebisho na maendeleo ya viwango vya kazi na maonesho ya TVET, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Franklin Rwezimula, alisema ushirikiano huo utaimarisha maendeleo ya TVET hasa katika kuzalisha nguvu kazi inayohitajika.

Amesema kuna maeneo mengi ya ushirikiano, ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu za pamoja za kitaaluma, kubadilishana wanafunzi na walimu, msaada wa rasilimali na teknolojia na huduma za utafiti na ushauri katika eneo la TVET.

Bw Rwezimula pia amewahamasisha Watanzania kuchangamkia fursa hiyo kwa kujenga ushirikiano imara, kubainisha maeneo yenye maslahi ya pamoja, na kuandaa mipango ya pamoja itakayoifanya TVET kuwa mstari wa mbele katika maendeleo endelevu ya kiuchumi.