Kongamano la kimataifa la Dakar juu ya amani na usalama barani Afrika lafunguliwa
2023-11-28 14:04:42| cri

Kongamano la tisa la kimataifa la Dakar juu ya amani na usalama barani Afrika lilifunguliwa Jumatatu huko Diamniadio, karibu na Dakar, mji mkuu wa Senegal. Rais Macky Sall wa Senegal na mwenzake wa Mauritania Mohamed Ould Ghazouani walishiriki kwenye mkutano huo.

Washiriki takriban 400 wakiwemo watoa maamuzi wa kiraia na kijeshi, wataalamu na watafiti barani Afrika, wanashiriki kwenye kongamano hilo lenye kauli mbiu ya “Uwezo na suluhu za Afrika katika kukabiliana na changamoto za kiusalama na ukosefu wa utulivu wa kitaasisi”.

Akihutubia kwenye ufunguzi wa mkutano huo Sall alisema Afrika inapata maendeleo kwenye njia ya kidemokrasia, lakini bado inaathiriwa na kutokuwepo na utulivu wa kitaasisi. Alisema migogoro na kutokuwepo na utulivu wa kitaasisi imeiingizia Afrika hasara kubwa. Mapambano ya silaha yanavuruga kabisa jitihada za Afrika za kupata maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Afrika inapaswa kuacha majaribio ya mapinduzi ya kijeshi na kutilia maanani maendeleo.