Uingereza yatakiwa kuzingatia kwa makini madai ya nchi kadhaa ya kurejeshewa vitu vya kale vilivyoporwa
2023-11-28 15:03:22| cri

Jumba la makumbusho la Uingereza linalojulikana duniani linaitwa “alama ya wizi” kutokana na kuwa asilimia kubwa ya vitu zaidi ya milioni nane vinavyohifadhiwa katika jumba hilo, vinatoka katika nchi nyingine. Katika miongo kadhaa iliyopita, nchi nyingi zinaendelea kudai kurejeshewa vitu vya kale vilivyoporwa na Uingereza.

Waziri mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis Novemba 26 alifanya ziara nchini Uingereza. Alipohojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC alisema Ugiriki inataka Jumba la makumbusho la Uingereza kurudisha sanamu ya mawe ya hekalu la Parthenon. Amesema hakuna ubishi wowote kuhusu umiliki wa vitu hivyo, vinamilikiwa na Ugiriki na viliibiwa.

Uingereza ilikuwa nchi yenye makoloni mengi zaidi barani Ulaya. Jumba la makumbusho la Uingereza ni jumba linaloonesha historia yake ya ukoloni. Kuanzia vitu vya shaba vya Benin kutoka Nigeria hadi jiwe la Rosetta kutoka Misri, vitu vingi vinavyohifadhiwa katika jumba hilo ni ushahidi wa uporaji wa Uingereza katika nchi za nje. Kati ya vitu hivyo, pia kuna vitu elfu 23 vya kale vya China.

Kwa mujibu wa takwimu zisizo kamili kutoka UNESCO, vitu vya kale zaidi ya milioni 1.64 vya China viko katika nchi za nje, na jumba la makumbusho la Uingereza ni moja kati ya majumba yanayohifadhi vitu vingi zaidi vya kale vya China vilivyoibiwa. Maelezo ya vitu hivyo huwa yanaonesha “chanzo halali”, lakini ukweli ni kwamba chanzo cha vitu hivyo ni vita, wizi, manunuzi katika soko haramu, ambavyo vingi vilitokea katika kipindi cha miaka 100 hivi kuanzia vita vya kasumba vilivyotokea mwaka 1840 hadi kuasisiwa kwa Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1949.

Ili kurejesha vitu hivyo vilivyoporwa, nchi kadhaa ikiwemo China zimefanya juhudi kubwa, lakini Uingereza imekataa kurudisha vitu hivyo kwa kisingizio cha “kulinda usalama wa vitu vya kale”. Mwaka 1963, bunge la Uingereza pia lilirekebisha “Sheria ya Jumba la Makumbusho la Uingereza”, na kupiga marufuku kisheria kurudisha vitu vya kale.

Mwezi Agosti mwaka huu, vitu 2,000 hivi vinavyohifadhiwa katika jumba la makumbusho la Uingereza vilitoweka, hata baadhi yake vinauzwa kwenye mtandao wa Internet. Tukio hilo limelifanya jumba hilo kupoteza uaminifu, na uwezo wake wa kulinda usalama wa vitu vya kale unatiliwa shaka. Nchi nyingi ikiwemo China zimetoa tena mwito wa kuitaka Uingereza irejeshe vitu vya kale.

Vitu vya kale ni chombo kinachorithisha na kubeba utamaduni wa nchi na makabila, na chenye kumbukumbu nyingi za kihistoria na kiutamaduni. Katika miaka kadhaa iliyopita, nchi nyingi hazijasita kudai jumba hilo na serikali ya Uingereza kurejesha vitu vivyo, ili kulinda utamaduni wa nchi na makabila na kufilisi mabaki ya kikoloni, ambayo uhalisi wake ni sehemu ya kampeni ya kimataifa ya kupambana na ukoloni.