Kiongozi wa Nigeria kutetea kuongeza msaada wa fedha na teknolojia kwenye mkutano wa COP28
2023-11-29 14:42:23| cri

Rais Bola Tinubu wa Nigeria amepangiwa kutoa taarifa kwenye mkutano wa 28 wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) utakaofanyika tarehe 1 na 2 Desemba mjini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, ukiwa chini ya kauli mbiu “Ungana, Tenda, na Toa”, ambako atatoa wito wa kuongeza msaada wa fedha na teknolojia kwa nchi zinazoendelea ambazo zinakabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yalisemwa kwenye taarifa iliyotolewa Jumanne na msemaji mkuu wa rais wa Nigeria Ajuri Ngelale, ambapo amebainisha kuwa Tinubu atasisitiza msimamo wa Nigeria juu ya masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na nishati endelevu na utoaji fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Kwa mujibu wa msemaji, ujumbe wa rais wa Nigeria pia utajikita katika kuwawajibisha wafanyabiashara na taasisi husika, na kuonyesha jitihada za Nigeria juu ya vitendo vyake endelevu na vya kuwajibika.