Rais wa China atoa pongezi kwa mkutano wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina
2023-11-30 10:37:46| cri

Rais Xi Jinping wa China ametoa ujumbe wa pongezi kwa mkutano wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na watu wa Palestina uliofanyika jana kwenye Umoja wa Mataifa.

Rais Xi amesema suala la Palestina ni kiini cha suala la Mashariki ya Kati, na linahusiana na haki na usawa wa kimataifa. Suala sugu la mgogoro kati ya Palestina na Israel ni kwamba watu wa Palestina wanashindwa kutimiza haki halali ya kitaifa kujenga taifa kwa kujitegemea. Mzunguko wa mapigano kati ya Palestina na Israel umethibitisha kuwa njia pekee ya kutimiza usalama wa kudumu ni kushikilia msimamo wa usalama wa pamoja. Jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuchukua hatua ya dharura na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatakiwa kutekeleza majukumu, ili kufanya juhudi zote kusimamisha vita, kulinda usalama wa raia wa kawaida, kuzuia maafa ya kibinadamu. Juu ya msingi huo, kuanzisha tena mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel haraka iwezekanavyo na kutimiza haki ya kujenga taifa, kuishi na kurudi kwa watu wa Palestina haraka iwezekanavyo.

Rais Xi amesisitiza kuwa China siku zote inaunga mkono kithabiti shughuli ya haki ya watu wa Palestina kurejesha haki halali ya kitaifa. Utatuzi wa kimsingi wa suala la Palestina ni kujenga nchi huru ya Palestina yenye mamlaka kamili kwenye msingi wa mpaka uliowekwa mwaka 1967, Jerusalem Mashariki ikiwa ni mji wake mkuu. Pia amesema mahitaji ya kiuchumi na maisha ya watu ya Palestina yanatakiwa kuhakikishwa, jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuongeza msaada wa maendeleo na wa kibinadamu kwa Palestina.