Mawaziri wa Afrika wapitisha maamuzi ya kuhimiza maendeleo ya kidijitali, maendeleo ya kiuchumi
2023-11-30 08:46:33| CRI

Mawaziri wa Afrika wanaosimamia mawasiliano na tehama wamepitisha maamuzi mapya yenye lengo la kuharakisha mabadiliko ya kidijitali barani Afrika, kuinua maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kuongeza nafasi za ajira na kuboresha maisha ya watu katika bara zima.

Uamuzi huo ulipitishwa jumanne kwenye ufungaji wa mkutano wa tano wa Kamati Maalumu ya Kiufundi (STC) kuhusu Tehama (ICT) barani Afrika.

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Afrika (AU), imesema mawaziri hao wameeleza dhamira ya kukuza uhusiano kati ya mfumo wa kidijitali, mabadiliko ya tabia nchi, miundombinu na nishati ili kuongeza manufaa ya masuluhisho ya kidijitali.

Mawaziri hao pia wameahidi kupigania kupitishwa kwa Mkakati wa Mabadiliko ya Kidijitali kwa Afrika na Mpango wa Utekelezaji wake, kama mradi kuu wa Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063 kwenye Mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika utakaofanyika mwaka 2024.