Spika wa Kenya apiga marufuku suti ya Kaunda na mavazi mengine ya kitamaduni ya Kiafrika bungeni
2023-11-30 23:38:31| cri

Spika wa bunge la Kenya amepiga marufuku yale aliyoyaita mavazi yasiyofaa yanayovaliwa na wabunge, hata kupiga marufuku mavazi ya kitamaduni ya Kiafrika na suti za mtindo wa safari zinazopendelewa na Rais William Ruto.

Moses Wentang'ula aliwaambia wabunge Jumanne kwamba lazima wafuate sheria za mavazi ya bunge, akikemea "mitindo inayoibuka ambayo sasa inatishia kanuni za mavazi za bunge".

Alisema ile inayoitwa suti ya Kaunda iliyopendwa na marehemu rais wa Zambia Kenneth Kaunda, vazi la mtindo wa safari wakati mwingine likiwa koti lisilo na kola, ilipigwa marufuku, pamoja na "vazi la kitamaduni".

Ruto mara nyingi huvaa suti rasmi za kushona lakini sasa suti ya Kaunda ndio vazi lake analochagua kuvaa, na pia alivaa wakati wa ziara ya Mfalme Charles III iliyomalizika mapema mwezi huu.

Kwa mujibu wa Kanuni za Spika, “vazi linalofaa kwa wanaume maana yake ni koti, kola, tai, shati la mikono mirefu, suruali ndefu, soksi na viatu au sare za huduma”.

Kwa wanawake, sketi na nguo lazima ishuke chini ya magoti na blauzi zisizo na mikono ni marufuku. Wentang'ula alisema alifuatwa na wabunge kadhaa ambao walilalamikia kiwango cha mavazi cha baadhi ya wenzao.