Kampuni ya China zasaini makubaliano ya kuongeza usambazaji wa bidhaa za mtandao wa internet kwa Afrika Mashariki
2023-11-30 08:28:05| CRI

Kampuni ya FiberHome International Technologies ya China imetia saini makubaliano na kampuni ya CP Cables ya Kenya ili kuongeza usambazaji wa bidhaa za mtandao wa kasi wa internet katika soko la Afrika Mashariki.

Naibu ofisa mkuu mtendaji (CEO) wa FiberHome International Technologies Bw. Bruce Wang, amewaambia wanahabari mjini Nairobi kwamba kutokana na makubaliano hayo ya miaka miwili, kampuni ya CP Cables itakuwa msambazaji mkuu wa bidhaa zao nchini Kenya na Uganda.

Makubaliano hayo yatawezesha Afrika Mashariki kupata bidhaa za hali ya juu zitakazosaidia watumiaji kunufaika na internet ya kasi kwa bei nafuu.

Bw. Wang amesema kampuni ya FiberHome imejitolea kuunga mkono lengo la Kenya la kuweka mtandao wa fiber optic kote nchini ili kupanua ufikiaji wa mtandao wa internet wa njia pana.