Katika nia ya kuendeleza mchezo wa Wushu Kung Fu nchini Tanzania, Kituo cha Utamaduni wa China nchini Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa China, kinaendesha semina kwa makocha na wachezaji, kwa lengo la kuongeza hamasa.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wushu Kung Fu Tanzania, Sempay Gola Kapipi alisema semina hiyo imeandaliwa na Kituo hicho na kuhudhuriwa na wakufunzi mbalimbali, ambao watafundisha watu katika vituo mbalimbali.
“Tunahitaji mchezo huu uchezwe shuleni pia, kwa kuanzia tulitoa mafunzo katika Shule ya Sekondari Zanaki na baadaye kusambaa katika shule nyingine,” alisema Sempay Gola.
Semina hiyo inaongozwa na mkufunzi wa kimataifa Wu Dong, ambaye ni mkurugenzi na profesa wa Kituo cha Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa cha Chuo Kikuu cha Michezo cha Beijing, China.
"Yeye ni mkufunzi wa kimataifa wa Wushu Kung Fu, ambaye ametoa mafunzo katika nchi nyingi duniani, ujio wake hapa ni fursa ya kupanua wigo wa mchezo huu," alisema.
Semina hiyo ilimalizika jana tarehe 30 Novemba, ambapo zaidi ya vijana 100 wamenufaika nayo.