Ding Xuexiang ahudhuria na kuhutubia mkutano wa kilele wa G77+China kuhusu mabadiliko ya tabianchi
2023-12-03 21:24:42| CRI

Mjumbe maalumu wa rais Xi Jinping wa China Bw. Ding Xuexiang, ambaye pia ni naibu waziri mkuu wa China, amehudhuria na kuhutubia mkutano wa kilele wa kundi la G77 na China kuhusu mabadiliko ya tabianchi uliofanyika mjini Dubai.

Kwenye hotuba yake Bw. Ding amesema, rais Xi Jinping amesisitiza kwamba mfumo wa “kundi la G77 na China” ni jukwaa muhimu kwa ushirikiano kati ya nchi zinazoendelea. Amesema kuwa kuboresha usimamizi wa tabianchi duniani bado kunahitaji juhudi kubwa zaidi, na G77 na China zinatakiwa kutoa sauti ya pamoja na kulinda maslahi ya pamoja.

Bw. Ding amesema, Kundi la G77 na China zinapaswa kusukuma mbele maendeleo endelevu, kuunganisha mikakati yao ya maendeleo ya kijani, kusaidiana na kutafuta kwa pamoja njia mpya inayooanisha maendeleo na uhifadhi; Pande hizo mbili zinapaswa kulinda taratibu za pande nyingi, kulinda kithabiti Mktaba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na malengo na kanuni zilizothibitishwa na Makubaliano ya Paris; Pia zinatakiwa kushirikiana katika kutetea haki na usawa, kuhakikisha fedha za tabianchi zinapatikana, kusukuma mbele uundaji wa mfumo wa malengo ya kimataifa ya kukabiliana na tabianchi (GGA) upige hatua halisi, na kutumia ipasavyo Mfuko wa Hasara na Uharibifu.