Rais wa Guinea-Bissau aita mapigano "jaribio la mapinduzi"
2023-12-04 10:23:48| CRI

Rais wa Guinea-Bissau Umaro Sissoco Embalo amesema mapigano makali yaliyotokea usiku wa Alhamisi hadi Ijumaa wiki iliyopita huko Bissau kati ya walinzi wa Kitaifa na vikosi maalum vya Walinzi wa Rais ni "jaribio la mapinduzi" ambayo yameleta matokeo mabaya kwa wote waliohusika.

Embalo alisema hayo wakati alipokuwa akiongea na wanahabari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Osvaldo Vieira Jumamosi jioni baada ya kurejea akiwa anatokea Dubai, ambako alihudhuria mkutano wa hali ya hewa wa COP28.

Taarifa kwa vyombo vya habari kutoka kwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi ilisema kuwa saa mbili usiku wa Alhamisi, kikundi cha askari, wakiongozwa na kamanda wao Kanali Victor Tchongo, waliwaachilia watu waliokuwa wakihojiwa katika kituo cha polisi wakiwa na lengo la kumtorosha waziri wa fedha Souleiman Seidi. Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi, Tchongo na baadhi ya watu wake walikamatwa Ijumaa asubuhi na polisi.