Jeshi la Uganda lasema kuondolewa kwa vikosi vya Jumuiya ya EAC nchini DRC hakutaathiri operesheni dhidi ya ADF
2023-12-05 10:28:18| CRI

Jeshi la Uganda limesema hatua inayoendelea ya kuondoka kwa jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) haitaathiri operesheni ya pamoja dhidi ya magaidi wa ADF kati ya Uganda na DRC.

Msemaji wa jeshi la Uganda, Deo Akiiki, aliiambia Xinhua kwa njia ya simu Jumatatu kwamba jeshi la nchi hiyo lilikuwa na operesheni tofauti ijulikanayo kama Shujaa ambayo inawawinda waasi wa ADF mashariki mwa DRC.

Kulingana na Akiiki, jukumu la jeshi la kikanda linalojumuisha wanajeshi wa Uganda, Burundi na Sudan Kusini lilikuwa kuhakikisha kwamba hakuna uhasama wa waasi wa M23 dhidi ya raia wa Kongo. Akiiki alisema jeshi la kikanda liliidhinishwa na wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki huku Operesheni Shujaa imepitishwa na Uganda na DRC.

Wanajeshi wa Uganda chini ya Operesheni Shujaa wamekuwa DRC tangu Novemba 2021 na kwa pamoja na vikosi vya Kongo wameweza kuharibu kambi kadhaa za ADF.