AfCFTA yatoa fursa kwa Afrika kufuata sera za hali ya hewa
2023-12-05 10:26:25| CRI

Afisa mwandamizi wa Tume ya Kiuchumi ya Umoja wa Mataifa barani Afrika (UNECA) amesema makubaliano ya Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFTA) yametoa fursa kwa nchi za Afrika kufuata sera za hali ya hewa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatatu katika hafla iliyofanyika wakati wa mkutano wa mabadiliko ya tabianchi (COP28) unaoendelea huko Dubai, Falme za Kiarabu, mratibu wa Kituo cha UNECA cha Sera ya Biashara Afrika (ATPC) Melaku Desta, amesema kwa niaba ya katibu mtendaji wa UNECA, Claver Gatete, kwamba wanapojitahidi kutumia uwezo wa AfCFTA, ni muhimu kufanya kwa njia ambayo italinda mfumo wa ikolojia, kukuza nishati mbadala na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akibainisha mahitaji yanayokua ya kuzingatia athari kwa mazingira wakati bara hilo likielekea kwenye ushirikiano mkubwa wa kiuchumi na kuchukua hatua za kukabiliana na athari zozote mbaya, Delta alisema Afrika inaathiriwa vibaya na mabadiliko ya hali ya hewa licha ya kuchangia kiasi kidogo katika utoaji wa hewa chafu.

Kulingana na takwimu kutoka UNECA, bara la Afrika kwa sasa linachangia takriban asilimia 7 ya uzalishaji wa hewa chafu duniani kutoka kwenye hewa ya ukaa na gesi nyinginezo.