Ethiopia yaipongeza China kwa kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu nchini humo
2023-12-06 10:58:18| cri

Ethiopia imeipongeza serikali ya China kwa msaada wake katika kuboresha ujumuishi wa wanafunzi wenye ulemavu nchini Ethiopia.

Pongezi hizo zimetolewa katika hafla maalum iliyofanyika jana jumanne baada ya kukamilika kwa ujenzi wa shule ya Alpha kwa Wanafunzi Viziwi katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, ambayo imejengwa kwa ufadhili wa China. Hafla hiyo ilihudhuriwa na maofisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Ethiopia, wanadiplomasia wa China nchini Ethiopia, wawakilishi kutoka mashirika ya hisani ya kimataifa, na wanafunzi wa shule hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Wanawake na Masuala ya Kijamii wa nchi hiyo, Huria Ali ameishukuru serikali ya China, kampuni na mashirika ya hisani kwa kuendelea kusaidia makundi yaliyo hatarini nchini Ethiopia.

Naye Balozi wa China nchini Ethiopia, Zhao Zhiyuang amesisitiza matokeo chanya ya ushirikiano wa pande nyingi wa China na Ethiopia, na michango ya kijamii na kiuchumi inayonufaisha watu wa pande zote mbili.