Tanzania yaomba msaada wa kibinadamu kwa wahanga wa mafuriko na maporomoko ya udongo huku idadi ya vifo ikiongezeka hadi 65
2023-12-06 09:47:32| CRI

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa wito kwa jumuiya za kimataifa na za ndani kusaidia katika kutoa misaada ya kibinadamu kwa watu walioathiriwa na mafuriko na maporomoko ya udongo katika wilaya ya Hanang mkoani Manyara.

Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu imesema, Majaliwa alisema idadi ya waliofariki kutokana na maafa ya mvua zilizosababisha mafuriko na maporomoko ya udongo imefikia 65 hadi kufikia Jumanne asubuhi na zaidi ya watu 116 wamejeruhiwa.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Katesh, moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi, Majaliwa alisema ofisi yake imepewa jukumu la kuratibu misaada ya kibinadamu inayotolewa na mashirika ya ndani na nje ya nchi, wafanyabiashara na watu binafsi. Taarifa hiyo ilisema Waziri Mkuu pia alisimamia kazi ya ukarabati katika maeneo yaliyoathirika na kuahidi kuwa serikali itafanya kila iwezalo kurejesha maeneo hayo katika hali ya kawaida.

Siku ya Jumatatu, ofisi ya rais ilisema takriban watu 5,600 wameachwa bila makazi na zaidi ya hekta 750 za mazao ya shambani zimeharibiwa.