Kenya yazindua mpango wa utekelezaji wa kuimarisha usalama wa chakula
2023-12-06 09:45:48| CRI

Kenya Jumanne ilizindua Mpango wa Utekelezaji wa Mifumo ya Chakula na Matumizi ya Ardhi ya Kenya 2024-2030, ambao unalenga kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Katibu mkuu wa Wizara ya Taifa ya Maendeleo ya Mazao na Utafiti, Paul Ronoh, aliwaambia wanahabari mjini Nairobi wakati wa sherehe za kuadhimisha Siku ya Udongo Duniani, ambayo ilikuwa Jumanne, kwamba mkakati huo unatoa mwongozo wa kukuza kilimo cha uzalishaji na chenye tija, kupunguza upotevu wa chakula, kuongeza ujumuishi wa vijana wa jinsia zote na kijamii, na kulinda na kurejesha mazingira ya asili.

Ronoh amebainisha kuwa masuala haya ni muhimu katika kuhakikisha maendeleo endelevu, kuboresha usalama wa chakula, na ustawi wa jamii za Kenya. Alifichua kuwa uzalishaji wa chakula nchini humo hauendani na ongezeko la watu, jambo ambalo limelazimisha uagizaji wa bidhaa kutoka nje ili kuziba pengo hilo.

Alisema mkakati huo pia unatoa miongozo ya lishe bora ambayo inaweza kusaidia kupunguza adha ya utapiamlo.