Mkutano wa mawaziri wa kulinda amani wa UM wafunguliwa nchini Ghana ili kuimarisha amani duniani
2023-12-07 09:36:03| CRI

Mkutano wa Mawaziri wa Kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa wa 2023 umefunguliwa Jumatano ukiwa na madhumuni ya kutafuta suluhu ya changamoto zinazokabili shughuli za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa na kuzifanyia kazi ili kupata matokeo madhubuti ya kuimarisha ufanisi wa operesheni za kulinda amani duniani kote.

Mkutano huo uliwakutanisha zaidi ya wajumbe 600, wakiwemo mawaziri wa ulinzi na wa mambo ya nje, na maafisa wa ngazi za juu wa serikali na wa jeshi huko Accra, nchini Ghana.

Katika hotuba yake ya ufunguzi Makamu wa Rais wa Ghana Mahamudu Bawumia aliwakumbusha wajumbe wa mkutano huo umuhimu wa kuwa na mtazamo thabiti wa kuzuia migogoro, ikiwa ni pamoja na hatua zinazosaidia kutatua vyanzo vya migogoro vinavyoathiri utulivu wa jamii yoyote ya binadamu.

Katika mkutano huo wa siku moja, wajumbe walijadili mada mbalimbali, zikiwemo kulinda raia, mawasiliano ya kimkakati, usalama, afya ya kisaikolojia ya walinda amani, na jukumu la lazima la wanawake katika ulinzi wa amani.