Somalia yaungana na tume ya FAO kudhibiti nzige wa jangwani
2023-12-07 09:37:19| CRI

Somalia Jumatano ilijiunga na Tume ya Kudhibiti Nzige wa Jangwani katika Kanda ya Kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) na kuwa mwanachama wake wa 17.

FAO imesema Somalia imepata maendeleo makubwa tangu 2020 ya kujenga uwezo wa kitaasisi na kiufundi wa kudhibiti nzige kwa msaada kutoka kwa wakala na washirika wa chakula wa Umoja wa Mataifa.

Kiongozi wa timu ya FAO ya Nzige na Wadudu wengine wa Mimea wanaovuka mipaka na Magonjwa, Shoki AlDobai, alisema Somalia ni nchi muhimu ya kuzaliana kwa nzige, na kuwa nao katika Tume kutanufaisha sio Somalia tu bali nchi jirani pia kwa kuimarisha ufuatiliaji na kutoa onyo la mapema kwenye kanda hiyo.

Kwa mujibu wa FAO, eneo la kijiografia la Somalia, umuhimu wa kihistoria katika udhibiti wa nzige na michango kwa Tume inaifanya kuwa mhusika muhimu katika kupambana na nzige katika Pembe ya Afrika. Imesema uanachama wa Somalia katika Tume hiyo ni hatua ya kimkakati itakayosaidia kuboresha juhudi za kudhibiti nzige kwenye kanda hiyo.