Taasisi za elimu za China na Ethiopia zakubali kukuza maendeleo ya ujuzi katika teknolojia
2023-12-07 09:33:18| CRI

Chuo Kikuu cha Teknolojia na Elimu cha Tianjin, China (TUTE) na Taasisi ya Mafunzo ya Ufundi ya Ethiopia (TVTI) zimetia saini makubaliano ya ushirikiano ili kuimarisha ukuzaji wa ujuzi unaozingatia maendeleo ya teknolojia.

Makubaliano hayo, yaliyotiwa saini Jumanne katika Karakana ya Luban ya Ethiopia inayofadhiliwa na China kwenye majengo ya TVTI huko Addis Ababa, yataongeza zaidi uwezo wa Karakana ya Luban ya Ethiopia.

Mkurugenzi mkuu wa TVTI, Biruk Kedir, alisema wakati wa hafla hiyo kuwa makubaliano hayo ni mfano tosha wa dhamira ya China katika kuboresha ujuzi wa teknolojia na uhandisi katika nchi hiyo. Wakati wa hafla hiyo, TUTE ilichangia vifaa vya kiteknolojia na vifaa vya uvumbuzi vinavyohitajika zaidi kwa TVTI.

Mwenyekiti wa Bodi ya TUTE Zhang Jingang amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu kwa China na Ethiopia kutekeleza mkakati wa kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja kwa kushirikiana katika elimu ya ufundi na kutekeleza miradi ya Mpango wa Ukanda Mmoja Njia Moja nchini humo.