Rais wa China akutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya
2023-12-07 14:24:08| cri

Rais Xi Jinping wa China leo hapa Beijing amekutana na mwenyekiti wa Baraza la Ulaya Charles Michel na mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ambao wako nchini China kuhudhuria mkutano wa 24 wa viongozi wa China na Umoja wa Ulaya.

Rais Xi amesema, tangu mwishoni mwa mwaka jana baada ya ziara ya viongozi hao wa Umoja wa Ulaya nchini China, uhusiano kati ya China na Ulaya umeonesha mweleko mzuri wa maendeleo, hali inayoendana na maslahi ya pande mbili na matarajio ya watu wao. Amesema, China na Ulaya zinapaswa kufanya juhudi kwa pamoja ili kudumisha mwelekeo huo mzuri.

Rais Xi ameainisha kuwa, huu ni mwaka wa 20 tangu China na Ulaya zianzishe Uhusiano wa Wenzi wa Kimkakati wa Pande Zote. Amesema China na Ulaya zinapaswa kuendelea kuinua kiwango cha kuaminiana kisiasa, kukusanya maoni ya pamoja ya kimkakati, kuimarisha uhusiano wa maslahi, na kupanua mazungumzo na ushirikiano, ili kunufaisha watu wa pande hizo mbili. Pia amesema China na Ulaya zinatakiwa kukabiliana kwa pamoja na changamoto zinazokabili dunia, na kushirikiana katika kuhimiza utulivu na ustawi wa dunia.