Rais wa Tanzania Samia Suluhu akagua eneo lililokumbwa na mafuriko na maporomoko ya udongo
2023-12-08 10:07:21| CRI

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Alhamisi alisafiri kwenda mkoani Manyara kukagua uharibifu uliosababishwa na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyotokea Jumapili katika wilaya ya Hanang mkoani humo.

Akitoa taarifa kwa Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama, alisema idadi ya watu waliofariki katika mafuriko hayo imeongezeka kutoka 69 siku ya Jumatano hadi 76 na kuongeza kuwa mafuriko hayo yamesababisha zaidi ya watu 5,600 kukosa makazi, na mazao 750 ya shambani yameteketea huku mifugo mingi ikifa. Alibainisha kuwa timu ya maafisa 1,285 kutoka idara za ulinzi na usalama wanaendelea kutafuta miili zaidi.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika mji wa Katesh ambao ni moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi, rais Samia amewataka wakazi wa mkoa wa Manyara kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu ambacho kinaweza kusababishwa na kuzorota kwa huduma ya maji baada ya vyanzo vya maji kuharibika. Pia aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi katika maeneo yaliyoathirika.