Rais wa Ushelisheli atangaza kuwa nchi yake inaingia kwenye hali ya dharura
2023-12-08 10:13:02| CRI

Kutokana na mlipuko wa ghala lenye baruti la kampuni moja ya ujenzi, na mafuriko yanayosababishwa na mvua inayoendelea nchini humo, rais Wavel Ramkalawan wa Ushelisheli ametangaza kuwa nchi yake inaingia kwenye hali ya dharura.

Ikulu ya nchi hiyo imetoa taarifa ikisema, mlipuko huo wa ghala umeleta uharibifu mkubwa kwenye eneo la viwanda la Providence na sehemu nyingine zilizoko karibu nalo, na mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa pia yameleta uharibifu mkubwa. Kwa maana hiyo watu wote wanatakiwa kukaa nyumbani isipokuwa wafanyakazi wa sekta muhimu za huduma na watu walioko safarini. Mbali na hayo, shule zote nchini humo zinafungwa kwa muda.

Habari zimesema kazi ya uokoaji bado inaendelea kufanyika kwenye eneo la tukio la mlipuko, na uchunguzi juu ya chanzo cha tukio hilo bado unaendelea.