AU na mashirika ya UM yaomba hatua za haraka zichukuliwe ili kumaliza baa la njaa barani Afrika
2023-12-08 10:10:55| CRI

Umoja wa Afrika na mashirika ya Umoja wa Mataifa Alhamisi yalitoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kumaliza baa la njaa barani Afrika ambapo karibu watu milioni 282, sawa na asilimia 20 ya watu wote hawana lishe bora.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, Tume ya Umoja wa Afrika, Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa barani Afrika, na Mpango wa Chakula Duniani walisema katika ripoti ya pamoja iliyopewa jina la “Muhtasari wa Kanda ya Afrika wa Usalama wa Chakula na Takwimu za Lishe na Mienendo 2023” kwamba idadi ya watu wenye lishe duni imeongezeka hadi milioni 57 tangu janga la UVIKO-19 lianze.

Mashirika hayo yameongeza kuwa wito wa kuchukua hatua kubwa zaidi unasalia kuwa wa kweli kutokana na makadirio ya kiwango cha chini cha ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei wa jumla na bei ya chakula, na kupanda kwa gharama za kukopa katika soko la ndani na kimataifa tangu 2022.

Ripoti hiyo ilisema kuzorota kwa hali ya usalama wa chakula na kukosekana kwa maendeleo kuelekea malengo ya lishe ya kimataifa ya Shirika la Afya Duniani kunalazimisha nchi kuongeza juhudi za kufikia dunia isiyo na njaa na utapiamlo ifikapo mwaka 2030.