Kuanzia Novemba 25 mpaka kesho Desemba 10, dunia inaadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia. Hatua hii ilifikiwa baada ya kuona wanawake wananyimwa nafasi ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Siku hizi 16 zinaanza Novemba 25 kwa kuadhimisha Siku ya Kupinga Ukatili na Unyanyasaji dhidi ya Wanawake, na kukamilika Desemba 10 ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu. Wanawake na wasichana ni kundi ambalo kiukweli limekuwa likiwekwa nyuma, ama tunaweza kusema ni kundi ambalo limekuwa likinyimwa fursa mbalimbali za kujiendeleza kiuchumi, kielimu, ujuzi, na hata katika suala zima la ajira. Mara nyingi katika kipindi hiki tumekuwa tukizungumzia jinsi wanawake wanavyojitahidi kupambana na mfumo dume ili kupata fursa sawa na wanaume katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
Vuguvugu ya siku hizi 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia zilianza mwaka 1989 baada ya mauaji ya "Mountreal," ambapo zaidi ya wanawake 14 waliuawa na wengine 13 kujeruhiwa vibaya. Wanawake hao walikuwa wanaharakati waliokuwa wanapigania haki yao ya kuwa wahandisi na wasomi, yaani wataalamu. Sasa katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake leo hii tutaangazia Siku hizo 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.