Nigeria yapiga hatua kubwa kuelekea kuzalisha mafuta yaliyosafishwa
2023-12-11 10:38:28| cri

Nigeria imetoa mapipa milioni ya mafuta ghafi kwa kiwanda kikubwa kipya cha kusafisha mafuta nchini humo, ikiwa ni alama muhimu katika mchakato wa nchi hiyo kuelekea kuwa na uwezo wa kuzalisha mafuta yenyewe.

Kwa miaka mingi Nigeria yenye utajiri mkubwa wa mafuta haikuwaza kuzalisha mafuta yaliyosafishwa, hali iliyoifanya nchi hiyo kuagiza mafuta yaliyosafishwa na kuongeza gharama za ziada.

Utoaji wa mapipa milioni moja ya kwanza ya mafuta ghafi utafuatiwa na mapipa milioni tano zaidi, ambayo yataruhusu kiwanda kuanza kutoa mafuta hayo.

Mafuta yatakayoanza kuzalishwa ni pamoja na dizeli, mafuta ya ndege na gesi miminika (LPG) kabla ya kuendelea na uzalishaji wa petroli. Tajiri mkubwa barani Afrika na mkuu wa kampuni ya Dangote, Bw. Aliko Dangote, amesema lengo katika miezi ijayo ni kuimarisha kiwanda hicho hadi kiwe na uwezo wake kamili. Kampuni inajivunia kuwa hatimaye itaweza kutoa kwa 100% mahitaji ya Nigeria ya bidhaa zote za mafuta yaliyosafishwa na ziada ya kuuza nje.