Dk Kijaji kuongoza Baraza la Mawaziri la AfCFTA kwa mwaka mmoja
2023-12-11 23:33:54| cri

Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania, Dk Ashatu Kijaji, amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na biashara katika Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA) kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Desemba 7. Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Dar es Salaam kikiongozwa na Dk Kijaji, kilipitisha Itifaki ya AfCFTA kuhusu Mchango wa Wanawake na Vijana kwenye Biashara barani Afrika.

Dk Kijaji aliongoza kikao cha 12 cha Baraza la Mawaziri wa AfCFTA Desemba 7, kilichofanyika sambamba na mkutano wa pili wa AfCFTA wa Wanawake Biashara (CWT), ambao ulianza Desemba 6 na kuhitimishwa Desemba 8. Itifaki hiyo kuhusu Wanawake na Vijana katika Biashara, ilikamilishwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ni mhamasishaji Mkuu na Kiongozi wa Wanawake na Vijana katika Biashara barani Afrika.