Katibu Mkuu wa UM asikitishwa na Baraza la Usalama la Umoja huo kushindwa kufikia makubaliano ya kusimamisha mapigano Gaza
2023-12-11 08:59:26| CRI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelitaka Baraza la Usalama la Umoja huo kuchukua hatua za kuepuka mgogoro wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, na kurejea tena ombi lake la kusitisha mapigano.

Guterres amesema hayo katika Jukwaa la Doha lililofanyika Qatar, siku mbili baada ya Marekani kutumia kura yake ya veto wakati wa mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzuia kupitishwa kwa azimio linalotaka kusimamisha mapigano mara moja katika Ukanda wa Gaza.

Azimio hilo, lililopendekezwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), lilipata kura 13 za ndio, huku Uingereza haikupiga kura, na Marekani kupiga kura turufu.

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amesema hatua hiyo ya Marekani inakubaliana na uhalifu wa kivita unaofanywa na jeshi la Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Naye mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Balozi Zhang Jun amesema mapigano yaliyodumu kwa miezi miwili katika Ukanda wa Gaza yamesababisha uharibifu mkubwa na vifo vya raia wasio na hatia, na yanapaswa kusimamishwa mara moja.