Wataalamu wa nyuklia wakutana nchini Kenya kuboresha utafiti katika teknolojia ya nyuklia
2023-12-12 08:44:39| CRI

Mkutano wa siku nane wa wataalamu wa nyuklia umeanza jana mjini Nairobi, Kenya, kwa lengo la kujadili njia za kuboresha utafiti katika teknolojia ya nyuklia.

Mkutano huo umekutanisha pamoja zaidi ya wataalam 100 wa nyuklia, mashirika ya utafiti na wasomi kutoka Afrika ili kutathmini njia za kutumia sayansi na teknolojia ya nyuklia kusaidia kukabiliana na changamoto kubwa ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, usalama wa nishati na changamoto za kiafya.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo, naibu mkurugenzi mkuu na mkuu wa idara ya nishati ya nyuklia katika Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) Mikhail Chudakov amesema, barani Afrika, nchi nyingi zinapanga kutekeleza miradi ya kitaifa ya utafiti wa nyuklia ili kuboresha sekta zao za afya, viwanda na uzalishaji wa kilimo.

Amesema IAEA inaunga mkono kwa kina kwa nchi wanachama katika kuendeleza miradi ya utafiti wa nyuklia ikiwemo msaada katika kuanzisha miundombinu ya nyuklia, ambayo ni changamoto kubwa inayozikabili nchi zinazotumia teknolojia ya nyuklia kwa mara ya kwanza.