Majanga ya asili yaathiri watu milioni 407 barani Afrika
2023-12-12 08:43:19| CRI

Kamati ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa (UNECA) imesema majanga ya asili yameathiri jumla ya watu milioni 407 barani Afrika kati ya mwaka 2000 hadi 2022, kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha mgogoro wa kibinadamu katika bara hilo.

Katika taarifa yake iliyotolewa jana jumatatu, UNECA imesema, matukio hayo yamewafanya watu milioni 4.2 kukosa makazi, huku watu 53,610 wakipoteza maisha na kujeruhi wengine 52,205.

Kamati hiyo imesema, mabadiliko ya tabianchi barani Afrika yanakwamisha juhudi za kuondokana na umasikini, na katika baadhi ya maeneo, kuharibu maisha ya mamilioni ya watu ambao wanategemea kilimo na biashara ndogondogo.