Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lalaani vurugu zinazoendelea nchini Sudan Kusini
2023-12-12 08:42:21| CRI

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali vurugu zinazoendelea katika Jimbo la Warrap nchini Sudan Kusini na kusini mwa eneo la Abyei, ambazo zimesababisha vifo vya watu kadhaa tangu mwezi uliopita.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, nchi wajumbe wa Baraza la Usalama wameonesha wasiwasi mkubwa juu ya kuendelea kuwepo kwa vikosi pamoja na makundi ya wapiganaji huko Abyei, eneo linalogombaniwa na Sudan na Sudan Kusini, na kusisitiza kuwa Abyei inapaswa kuwa eneo lisilo na silaha bila ya kuchelewa.

Wajumbe hao wameunga mkono wito uliotolewa na mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, Nicholas Haysom, wakisisitiza haja ya serikali ya mpito ya Sudan Kusini kuchunguza mauaji na mashambulizi dhidi ya raia huko Warrap na Abyei, kudhibiti vurugu na kupunguza mvutano kati ya jamii zilizoathirika.

Aidha wamesisitiza jukumu muhimu linalotakiwa kutekelezwa na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa huko Abyei katika kulinda raia, kuunga mkono mazungumzo na maafikiano ya jamii, na kuhimiza utimizaji wa amani, usalama na utulivu huko Abyei na maeneo makubwa zaidi.