Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Operesheni za Amani Jean-Pierre Lacroix ameeleza kufurahishwa na mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Ngazi ya Mawaziri wa Ulinzi wa Amani wa mwaka 2023 uliomalizika hivi karibuni mjini Accra, Ghana, ambapo nchi nyingi wanachama, ikiwemo China, zilitoa ahadi muhimu.
Akihojiwa na Shirika la Habari la China Xinhua, Bw. Lacroix ameeleza kuridhishwa kwake na ahadi zilizotolewa katika maeneo kadhaa ikiwemo askari wa miguu, vikosi vya mwitikio wa haraka, idara za uhandisi, na idara za kupambana na vifaa milipuko.
Ameipongeza China uungaji mkono wake, ikiwa ni mchangiaji wa pili wa kifedha katika operesheni za ulinzi wa amani na ahadi yake ya kuimarisha uwezo na utayari wa vikosi vya kulinda amani.
Amesema ahadi ya China ya kuendelea kupeleka askari na ahadi nyingine muhimu katika mafunzo, kuwa mwenyeji wa mafunzo ya kimataifa, na kuunga mkono ushirikiano wa kikanda wa ulinzi wa Amani ni za muhimu sana.