Maonyesho ya 23 ya biashara ya EAC yafungua masoko mapya kwa wafanyabiashara
2023-12-13 08:42:34| CRI

Ufunguzi wa Maonyesho ya 23 ya Biashara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Kampuni Ndogo na za Ukubwa wa Kati umefanyika ijumaa iliyopita katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura.

Taarifa iliyotolewa na makao makuu ya Jumuiya hiyo mjini Arusha, Tanzania imesema, maonyesho hayo yaliyoanza tarehe 5 mwezi huu na yanayotarajiwa kumalizika ijumaa wiki hii, yamevutia zaidi ya washiriki 1,000 kutoka nchi 7 wanachama wa EAC ambazo ni Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokraisa ya Kongo (DRC) na Uganda.

Makamu wa rais wa Burundi, Prosper Bazombanza amesema, maonyesho hayo ni ushuhuda wa maendeleo endelevu ya kiuchumi na maingiliano ya biashara kati ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo, na kuongeza kuwa, maonyesho hayo yanachukua nafasi kubwa katika kuondoa pengo la kiteknolojia kati ya wafanyabiashara katika kanda hiyo.