UM watoa wito wa kusitisha mapigano kwa sababu za kibinadamu nchini Sudan ili kuepuka janga la njaa
2023-12-14 08:54:17| CRI

Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa pande zote zinazohusika na mgogoro nchini Sudan kufikia makubaliano ya kusimamisha vita kwa sababu za kibinadamu ili kuwezesha nchi hiyo kuepuka janga la njaa.

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limesema katika taarifa yake kuwa, sehemu zinazokabiliwa na mapigano nchini Sudan ziko katika hatari ya kukabiliwa na janga la njaa itakapofika msimu wa mavuno mwaka ujao kama Shirika hilo litashindwa kupeleka msaada wa chakula mara kwa mara kwa watu waliokwama kwenye maeneo ya vita.

Shirika hilo limesema karibu watu milioni 18 nchini Sudan wanakabiliwa na njaa kali, ikiwa ni mara mbili zaidi ya idadi hiyo kwa mwaka jana.

Wakati huohuo, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetoa tahadhari kuhusu kuongezeka kwa ukosefu wa usalama wa chakula nchini Sudan, na kutaka hatua za haraka na za pamoja zichukuliwe ili kukwepa mgogoro wa kibinadamu.