Kenya yazindua mkakati wa kuimarisha biashara ya mtandaoni
2023-12-14 08:53:21| CRI

Kenya imezindua mkakati wa kitaifa wa biashara ya mtandaoni, ili kurahisisha sekta hiyo inayokua kwa kasi kufuatia ustawi wa uchumi wa kidijitali.

Katika uzinduzi huo, katibu wa Baraza la Mawaziri la Kenya anayeshughulikia mambo ya habari, mawasiliano na uchumi wa kidijitali Eliud Owalo, amesema mkakati huo unalenga kuifanya Kenya kuwa kitovu cha kikanda cha biashara ya mtandaoni, kuongeza biashara ya ndani na nje ya nchi na kuongeza mapato na ajira.

Amesema mkakati huo utaimarisha upatikanaji wa masoko ya kimataifa kwa bidhaa na huduma za Kenya, hasa kwa kampuni ndogo na za kati kupitia biashara ya mtandaoni.