Nchi za Afrika zajadili kuanzisha taasisi za kifedha za Umoja wa Afrika
2023-12-14 08:55:50| CRI

Mkutano wa mashauriano wa nchi za Afrika katika kuanzisha taasisi za kifedha za Umoja wa Afrika (AU) umefanyika mjini Lusaka, Zambia, na kutoa wito kwa washiriki kuunda mfumo utakaoongeza kasi ya kuanzishwa kwa taasisi hizo.

Mkutano huo wa siku tatu umekutanisha mawaziri wa fedha kutoka nchi wanachama, wajumbe kutoka Benki Kuu za nchi hizo, idara za Umoja wa Afrika, jamii za kiuchumi za kikanda na wenzi wa maendeleo, kwa lengo la kujadili changamoto za kiuchumi na kisiasa zinazokwamisha nchi wanachama kusaini na kuidhinisha idara za kisheria zinazohitajika kwa ajili ya kuanzisha taasisi za kiuchumi.

Waziri wa Fedha na Mipango wa Zambia Situmbeko Musokotwane amesisitiza umuhimu wa kuanzisha taasisi hizo, akisema zina nafasi kubwa katika kuunga mkono matumizi mazuri ya Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFTA). Amesema mkutano huo umefanyika katika wakati sahihi na ni muhimu kwa kuwa Eneo la Biashara Huria la Afrika linalenga kuondoa vizuizi vya kibiashara na kuboresha biashara ya ndani ya Afrika.