Ukame wapungua nchini Kenya kufuatia mvua za El Nino
2023-12-15 08:41:05| CRI

Mamlaka ya Kudhibiti Ukame nchini Kenya (NDMA) imesema, mvua za El Nino zinazoendelea kunyesha nchini humo zimebadili hali ya ukame katika maeneo ya jangwa na nusu jangwa nchini humo.

Katika taarifa yake, Mamlaka hiyo imesema kaunti 20 kati ya 23 zilizoathiriwa vibaya na ukame zimerejea kikamilifu katika hali ya kawaida, huku kaunti nyingine tatu zikiwa katika mwelekeo wa kufufuka.

Taarifa hiyo imesema, kesi za utapiamlo katika maeneo hayo zimepungua, huku hali ya lishe ikiendelea kuwa ya utulivu na inatarajiwa kuboreka kutokana na mvua hizo.

Hata hivyo, Mamlaka hiyo imesema, ingawa mgogoro wa ukame umemalizika nchini humo, maeneo ya jangwa na nusu jangwa, ikiwemo Marsabit, Isiolo, Samburu, Wajir, Garissa na Mandera, yaliyoko kaskazini mwa Kenya, yamekumbwa na mafuriko makubwa yaliyosababisha vifo na watu na wanyama kukosa makazi.