China yatoa wito kwa pande zote nchini Sudan Kusini kuweka mazingira mazuri kwa uchaguzi mkuu
2023-12-15 08:38:14| CRI

Naibu mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Balozi Dai Bing ametoa wito kwa pande zote nchini Sudan Kusini kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini humo.

Balozi Dai amesema hayo alipohutubia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu suala la Sudan Kusini. Amesema katika siku za hivi karibuni, Sudan Kusini imetekeleza kikamilifu makubaliano ya kutatua mgogoro, kutangaza sheria ya uchaguzi, kuunda upya idara za serikali na kupata maendeleo makubwa. Amesema Sudan Kusini inapanga kufanya uchaguzi mkuu mwezi Desemba mwaka ujao, ambao utaathiri hali ya jumla ya maendeleo na utulivu wa nchi hiyo, na China inatoa wito kwa pande zote nchini humo kutoa kipaumbele kwa maslahi ya nchi na watu wake, na kuondoa tofauti kupitia mazungumzo.

Pia amesisitiza kuwa, China inaunga mkono Tume maalumu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) ikishirikiana na Umoja wa Afrika na Shirika la Maendeleo ya Kiserikali la nchi za Afrika Mashariki (IGAD) kuendelea kutoa misaada katika mchakato wa kisiasa nchini humo.