Mawaziri wa mambo ya nje wa China na Kenya wapeana pongezi kuadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kibalozi
2023-12-15 13:55:42| cri

Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi na mwenzake wa Kenya Musalia Mudavadi wametumiana salamu za pongezi kwa njia ya simu wakati nchi zao zinaadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kibalozi.

Bw. Wang amesema tangu China na Kenya zianzishe uhusiano wa kibalozi miaka 60 iliyopita, nchi mbili siku zote zimekuwa zikitendeana kwa usawa, kushikamana na kushirikiana, kutafuta maendeleo kwa pamoja, na zimekuwa marafiki wakubwa, wenzi wazuri wanaoaminiana.

 Amesema Ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” kati ya China na Kenya umepata maendeleo makubwa, ukiongoza katika ushirikiano kati ya China na Afrika, kuweka mfano wa kuigwa na kutoa mchango mkubwa katika kujenga jumuiya yenye hatma ya pamoja kati ya China na Afrika.

Kwa upande wake Bw. Mudavadi amesema China ni moja kati ya nchi zilizoanzisha mapema zaidi uhusiano wa kibalozi na Kenya, na Kenya na China zinaaminiana, kuheshimiana, huku uhusiano kati ya nchi hizi mbili ukiwa karibu na wa kirafiki. Kabla ya hapo, wakati Rais William Ruto wa Kenya alipokutana na mwenzake wa China Bw. Xi Jinping kwenye mkutano wa 3 wa kilele wa Ushirikiano wa kimataifa wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, walihimiza uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote kati ya nchi mbili upige hatua zaidi.

Amesema anapenda kufanya juhudi pamoja na Bw. Wang kutekeleza makubaliano muhimu yaliyofikiwa na  wakuu wa nchi hizo mbili, na kutimiza kihalisi mpango mzuri wa uhusiano kati ya nchi mbili.