Tanzania yapata nafasi ya obiti na kufungua njia ya kurushwa kwa satelaiti ya kwanza
2023-12-18 11:01:39| cri

Tanzania imepata nafasi muhimu katika obiti na kufungua njia ya kurusha satelaiti yake ya kwanza katika anga ya juu.

Mafanikio hayo ya kihistoria yaliyotangazwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, yanaashiria hatua kubwa ya nchi ya kusonga mbele katika malengo yake ya anga ya juu.

Habari hizi zinakuja baada ya Bw Nnauye kuwahakikishia Watanzania mwezi Julai dhamira isiyoyumba ya serikali ya kurusha satelaiti kuu ya nchi ndani ya mwaka, akisema wanajiamini na kwa sasa wanaweka msingi.

Uwezo wa satelaiti ya Tanzania ni mkubwa. Sekta kama vile mawasiliano, kilimo, usimamizi wa maafa, na viwanda washirika zitanufaika sana kutokana na uwezo wake. Zaidi ya hayo, teknolojia hii itatumika zaidi ya hapo ikiingia kwenye utafutaji wa maliasili na sekta nyingine muhimu za kiuchumi.

Katika bara zima la Afrika, ni mataifa machache tu yanayotumia uwezo wa teknolojia ya satelaiti. Misri inaongoza kwa satelaiti tisa katika obiti, ikifuatiwa na Afrika Kusini (nane), Algeria (saba), na Nigeria (sita). Nyingine kama Morocco, Ghana, Kenya, Rwanda, na Mauritius zimejiunga na mataifa yanayosafiri angani.