Rais Ruto asema hana udhibiti wa mambo yanayosababisha kuongezeka kwa gharama ya maisha
2023-12-18 11:01:10| cri

Rais William Ruto amesema kuwa mambo yanayozidisha gharama kubwa za maisha yako nje ya uwezo wake.

Katika mahojiano ya pamoja na wanahabari Jumapili jioni, Dkt Ruto alisema Wakenya watalazimika kusubiri kwa muda hadi kiwango cha dola/shilingi kiwe kizuri, akisisitiza kuwa hakuna muujiza utakaotokea.

Ameendelea kubainisha kwamba bei ya mafuta haidhibitiwi na serikali ya Kenya, bali inadhibitiwa na wazalishaji.

Alisema serikali ilibidi kuchukua maamuzi magumu na yenye maumivu, lakini aliongeza kuwa ni bora kuchukua maamuzi haya leo kuliko kuwaweka Wakenya katika dhiki ya madeni. Hata hivyo amesema alijua kabla ya kuchaguliwa kuwa isingekuwa rahisi.

Pia alisisitiza kuwa bei ya mafuta nchini Kenya ni sawa na ya Uganda na Tanzania kwa sababu nchi zote hizi zinanunua mafuta kutoka kwa wazalishaji wale wale.