Kenya yachunguza shughuli za kundi jipya huku kukiwa na mgogoro wa kidiplomasia na DRC
2023-12-18 08:27:28| CRI

Kenya imeanzisha uchunguzi kuhusu shughuli za kundi jipya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) lilioanzishwa mjini Nairobi ambalo limezua mgogoro wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Ijumaa iliyopita raia wa DRC wakiwemo waasi wa M23, ambao wameteka eneo la mashariki mwa nchi hiyo, na Bwana Corneille Nangaa, mwenyekiti wa zamani wa tume ya uchaguzi nchini DRC, walizindua Muungano wa Mto Kongo mjini Nairobi, nchini Kenya.

Bwana Nangaa aliwaambia wanahabari wakati wa uzinduzi wa kundi hilo kuwa pia linalenga wanachama kutoka jeshini, mashirika ya kiraia, na jumuiya ya diaspora, na linasukumwa na nia ya kuiokoa DRC kutoka kwenye hatari na kurejesha heshima ya watu wa Kongo.

Bwana Nangaa ambaye aliambatana na kiongozi wa kundi la M23 Bertrand Bisimwa, amesema kuundwa kwa muungano huo kulitokana na "kutekwa nyara kwa mchakato wa uchaguzi".

Serikali ya DRC imewaita mabalozi wake kutoka Tanzania ambayo ni mwenyeji wa makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Kenya kwa ajili ya mashauriano kuhusu jambo hilo.