Tanzania kuandaa michuano ya CHAN 2024 pamoja na Kenya na Uganda
2023-12-19 13:48:26| cri

Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) Wallace Karia ametangaza kuwa Tanzania itaandaa michuano ya Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024 pamoja na Kenya na Uganda.

Oktoba Mosi, Serikali ya Kenya iliidhinisha mipango ya kuandaa michuano hiyo itakayoshirikisha timu 16, kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani, lakini Karia ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alisema tukio hilo sasa litafanyika hadi nje ya ukanda mkubwa wa Afrika Mashariki.

“Mwaka ujao Septemba, tumepewa haki ya kuandaa CHAN katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda na kila taifa pamoja na Zanzibar watatoa uwanja mmoja kwa ajili ya mashindano hayo,” alisema Karia katika mkutano mkuu wa mwaka wa TFF uliofanyika Iringa Tanzania.

Algeria ilikuwa mwenyeji wa michuano ya mwisho ya CHAN mwezi Januari na Februari 2023 ambapo Senegal ilishinda taji hilo kwa kuwafunga wenyeji kwa mikwaju ya penalti katika fainali.