Mwanariadha wa zamani wa Kenya afariki dunia wakati akimuokoa mbwa wa muajiri wake
2023-12-19 22:47:46| cri

Mwanariadha wa zamani wa Kenya Josephat Kibet Ngetich alikufa maji alipokuwa akijaribu kumwokoa mbwa aliyeanguka kwa bahati mbaya kwenye bwawa siku ya Jumanne, wiki iliyopita katika makazi ya mwaajiri wake nchini Mexico.

Familia yake huko Kenya iliarifiwa kuhusu kifo cha mpendwa wao Alhamisi, wiki iliyopita na kuzua taharuki kubwa katika kijiji cha Taabet, wadi ya Chesoen, eneo bunge la Bomet ya Kati, kaunti ya Bomet.

Kifo chake kimeiacha familia yake katika mfadhaiko na haijulikani ni kwa nini aliamua kuhatarisha maisha yake ili kuokoa mbwa.

Hata hivyo familia hiyo inasema haiwezi kukusanya Sh milioni tatu za Kenya zinazohitajika ili mwili urudishwe nyumbani.